Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, ujumbe kamili wa Ayatullah Alireza Arafi, Mkuu wa Hawza nchini Iran, kwa kozi ya mafunzo ya Mpango wa “Mfumo Kamili wa Fikra na Maisha ya Kijamii ya Kiislamu” ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
Kwa kuzitolea salamu roho za Mitume na Mawalii, hususan Khatamul-Anbiya (saww) na Khatamul-Awsiya (ajf), na kwa kuzitolea salamu roho takatifu ya Imam Khomeini (r.a.), roho safi za mashahidi adhimu wa Uislamu, Mapinduzi ya Kiislamu, vita na Ulinzi wa Tatu, hususan Kiongozi na Imam Shahidi na mpendwa (q.s.), nawasilisha salamu zangu za dhati pamoja na shukrani nyingi kwa waheshimiwa walimu, wanazuoni na wanafunzi wapendwa walioshiriki katika kozi ya juu ya Mfumo Kamili wa Fikra za Kiislamu, pamoja na waandaaji waheshimiwa wa kozi hii na Naibu Mkuu anayeheshimika wa Idara ya Utakaso na Malezi, katika ardhi tukufu ya mbinguni na karibu na kaburi tukufu la Hadhrat Thamin al-Hujaj (as).
Nilitamani kupata fursa ya kwenda kumzuru Imam huyo mkubwa (as), pamoja na kutembelea kaburi tukufu la Kiongozi Shahidi (r.a.), ili kwa karibu nitoe heshima, taadhima, pongezi na shukrani zangu, lakini vikwazo vilininyima fursa hiyo.
Natumia fursa hii kukumbusha kwamba; katika mkusanyiko wa nyaraka, mipango na programu za mageuzi ya Hawza, na katika mwelekeo wa kukuza, kuendeleza na kuifikisha Hawza katika ubora wa “Hawza inayoongoza na bora,” Mpango wa Mfumo Kamili wa Fikra za Kiislamu una nafasi muhimu. Lengo lake ni kuwafahamisha wanafunzi wapendwa, hususan wale walio katika ngazi ya masomo ya Sat-h, kuhusu mfumo kamili wa fikra za Kiislamu na mti mpana wa maarifa ya kidini na kimapinduzi, kwa mtazamo wa wanafikra mashuhuri wa kisasa wa Hawza na Maimamu wawili wa Mapinduzi, kwa mtazamo wa kiistaarabu na kimapinduzi.
Kukosekana au kudhoofika kwa mtazamo wa aina hii mpana, wa kiistaarabu na wenye kuleta uhai ndani ya mwanafunzi wa Hawza, mwalimu na mwanazuoni wa dini ni tatizo kubwa ambalo halipaswi kupuuzwa. Mipango kama huu, Mpango wa Wilaya na Mpango wa kusoma kazi za Shahidi Murtadha Mutahhari (r.a.), inalenga kurekebisha upungufu huu na kuziba pengo hili.
Ukweli ni kwamba, daima tumekuwa tukikabiliana na tafsiri pungufu, usomaji finyu, mitazamo isiyozingatia ustaarabu, pamoja na mitazamo inayotazama sehemu moja moja na yenye mipaka kuhusu Uislamu mtukufu na maarifa ya juu ya Mtume Mtukufu (saww) na Ahlul-Bayt wake watoharifu (as).
Hata hivyo, katika zama mpya, Hadrat Imam Khomeini (r.a.), Imam Shahidi Khamenei (r.a.), Allamah Tabatabai (r.a.), Shahidi Muhammad Baqir Sadr (r.a.), wanafunzi wao mashuhuri, pamoja na wanazuoni wakubwa wa Hawza, kwa mtazamo mpana na wa kustaarabisha kuhusu Uislamu mtukufu, waliwasilisha tafsiri hai, yenye kuleta uhai na kuchochea harakati kuhusu Uislamu. Fikra hii ilidhihirika kwa vitendo kwenye Mapinduzi matukufu ya Kiislamu, ikaunda ulimwengu mpya, na kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, chini ya uongozi wa Kiongozi Adhimu, Marajii wakuu, wanafikra na viongozi wa Hawza, mwangwi wa harakati hii ya kimaarifa utaendelea kusikika nchini Iran na duniani kote.
Mwishoni, ninawaomba wanazuoni na watu wa Hawza, hususan wanafunzi vijana wenye elimu na uwezo, ambao ni mitaji ya baadaye ya Hawza na Mapinduzi ya Kiislamu, waoneshe umuhimu na umakini kwenye masuala haya ya kimkakati, mipango ya mageuzi na Mpango wa Mfumo Kamili wa Fikra za Kiislamu, pamoja na kukuza maarifa na uelewa mpana, sambamba na kushiriki katika uwanja wa vitendo na kutekeleza majukumu katika nyanja za kiutamaduni, kijamii, kimahubiri na katika jamii.
Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awape nyinyi na wapendwa wote mafanikio katika njia hii tukufu na ngumu. Nawashukuru kwa dhati, ninawaombea na naomba radhi kwenu. Natumaini mtakuwa miongoni mwa wanaopata fadhila na upendeleo wa Mtukufu Imam Ridha (as) na Mtukufu Waliyyul-Asr (roho zetu ziwe fidia kwake).
Na mwisho wa dua yetu ni: Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu.
Alireza Arafi
Mkuu wa Hawza nchini Iran
Maoni yako